Sunday, July 7, 2013

WATAKA KUPATA MAFANIKIO MAISHANI?




Watu wanaofanikiwa kikweli kwa kupitia njia bora kabisa maishani ambayo inatokana na kufuata viwango vya Mungu na kuishi kupatana na kusudi la Mungu. Biblia inasema hivi kwa mtu anayetaka kupata mafanikio “Naye atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, uzaa matunda yake kwa majira yake, wala jani lake halinyauki”. (Zaburi 1:3).
Ingawa sisi si wakamilifu mbele za Mungu na tunafanya makosa lakini tunaweza kufanikiwa maishani. Kwa kusoma maandiko matakatifu (Biblia) inaweza kukusaidia ufikie lengo hilo, kwani kwa kusoma tunapata hekima ya Mungu. “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” Yakobo 3:17.
1.      KUWA NA MTAZAMO UNAOFAA KUHUSU PESA.
“Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi” (I Timotheo 6:10). Siku zote tatizo sio kuwa na pesa maana tunahitaji pesa ili kukidhi kupata mahitaji yetu ya kila siku na kutunza familia zetu pia.
Tatizo lililopo ni KUPENDA PESA. Maana katika kupenda pesa kwaweza kumfanya mtu kuanza kuiabudu pesa kama ndio Mungu wake na kuanza kusahau kumwabudu MUNGU aliyemuumba.
Watu ambao hutafuta kuwa matajiri ili wapate mafanikio nikimaanisha KUPENDA PESA wengi wao ingawa sio wote wamejikuta katika maumivu makali, Maana katika harakati zao za kutafuta pesa wengine kwa njia za kufanya Ufisadi kwa kuiba mali za uma, kuwadhulumu wajane, Yatima na hata wengine kwa kuwakata viungo walemavu wa ngozi (albino), wamekosa kuwa na Amani maishani mwao hivyo kukosa usingizi sit u kwa sababu ya kazi nyingi bali kwa kuwa na wasiwasi mioyoni mwao maana wamejitengenezea maadui katika familia zao, na hata miongoni mwa marafiki zao. “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi. Lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi”(Mhubiri 5:12).
            Zaidi ya kuwa bwana mkatili, kupenda pesa ni bwana mdanganyifu (Marko 4:19). Maana yake ni kwamba utajiri humwahidi mtu kupata furaha lakini haufanyi hivyo. Baada yake umfanya mtu atamani utajiri zaidi. Ebu soma nami katika kitabu cha Mhubiri 5:10. “Apendaye fedha hatashiba fedha, wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.
            Kifupi ni kwamba mtu anayependa pesa sana anajiumiza tu.Anavunjika moyo, anakatishwa tama au hata kujihusisha katika uhalifu Mithali 28:20 “Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka”.
            Ukarimu, Usafi wa maadili, Mahusiano mazuri pamoja na Mungu, Upendo na kuwa tayari kusamehe hayo ni mambo yanayoleta furaha na mafanikio maishani.
2.      KUWA NA ROHO YA UKARIMU.
“Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea”. Unapokuwa na Roho ya Ukarimu kwa watu wote walio na uhitaji na wasio nao unakuwa na furaha ya kudumu moyoni mwako maana unapowatendea mojawapo ya hao unakuwa unamtendea Mungu.
Mtafiti mmoja mara baada ya kufanya uchunguzi wa muda mrefu kuhusu afya, furaha, na kutokuwa na ubinafsi, mtafiti alibaini kwamba kutokuwa na ubinafsi na kuwasaidia wengine kunahusianishwa na maisha marefu, afya nzuri kimwili, kiakili, kijamii na kiroho lakini pia husaidia kupunguza kupatwa na kushuka kwa moyo.
Lakini pia watu wenye roho ya ukarimuhawapungukiwi na kitu chochote maishani. “Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa, Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe”. (Mithali 11:25). Hii inamaanisha kwamba  wale wote wanaofanya ukarimu toka moyoni na sio wale wanaojifanya ni wakarimu ili watu wawaone kuwa ni wakarimu huku wakitarajia siku moja na wao watawalipa fadhila zao. Sasa kwa wale walio na ukarimu wa moyoni sadaka zao hizo zinampendeza Mungu sana (Waebrania 13:16)
3.      SAMEHE KWA AJILI YA YESU.
Siku hizi watu wengi pale wanapoombwa  msamaha na wale waliowakosea usema mioyoni mwao kuwa NIMEKUSAMEHE LAKINI SITAKUSAHAU. Huo utakuwa ni msamaha wa kinafiki. Ebu niwaeleze jambo moja lililowahi tokea huko Afrika ya kusini enzi ubaguzi wa rangi mama mmoja aliyekuwa na na kijana wake ambaye kutokana na ukandamizaji wakati huo mtoto wake alitiwa mikononi mwa polisi kasha kutokana na mateso huko kizuizini alifia huko na mara baada ya kuundwa kwa tume ya ukweli na maridhiano huko Afrika ya kusini Chini ya Askofu Desmond Tutu askari polisi mmoja alikutwa na hatia ya kumuua kijana wa mama huyo, kesi ilipopelekwa mahakamani yule mama akaona hata polisi huyo atakapokutwa na hatia ya mauaji hawezi kumpata kijana wake, hivyo basi mama huyo alipoitwa na tume hiyo alieleza kuwa yeye yuko tayari kumsamehe askari polisihuyo wakati wa enzi za utawala wa makaburu na tena akasema kuwa kuanzia wakati huo yeye ndiye atakuwa sawa na kijana wake. Ni msamaha wa wa namna ya pekee sana na wa nadra sana mioyoni mwa wale waliopotelewa na wapendwa , au wazazi wao.
Katika ripoti moja ya Gazeti la The Gazette la Montreal, Canada inasema kwamba “Katika uchunguzi uliofanyiwa watu zaidi ya 4600 wenye umri ya kati ya miaka 18 hadi 30”,wachunguzi waligundua kwamba uhasama, kukata tama, na kutokuwa na fadhili hufanya mapafu yawe mabovu. Kwa kweli mambo hayo yanaweza kufanya mapafu ya mtu kuwa mabovu zaidi kuliko ya mvutaji wa sigara.
Kumbe kusamehe hakufanyi iwe rahisikushughulika na wengine tu bali pia unafaidisha Afya zetu.
Ili tuweze kusamehe zaidi ebu anza kujichunguza kwamba je, wakati mwingine huwa hauwakasirishi watu? Unafurahi wanapokusamehe?Kwa hiyo mbona hauwasamei wengine?. Hata kama kulikuwa na mtu aliyetaka kuiangamiza  roho yako kwa uchawi au kwa kukuwekea sumu kwenye chakula bado tunaambiwa ni sharti tuwarehemu.(Mathayo 18:21-35).
Tambua kuwa kujizuia sio udhaifu kuliko kulipiza ovu kwa ovu. Ebu soma kitabu cha Mithali 16:32 “Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa. Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji”.
4.      KUISHI KWA KUFUATA KANUNI ZA MUNGU.
“Maagizo ya BWANA ni ya adili, huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, huyatia macho nuru”. (Zaburi 19:8). Kwa kweli kanuni (sheria) za Mungu zinafaida kubwa sana kwetu wanadamu maana zinatulinda dhidi ya mazoea mabaya kama vile kutumia dawa za kulevya, pombe, ukosefu wa maadili na kutazama, kuona  au hata kusikiliza habari na picha zenye kuamsha hisia za ngono. (II Wakorintho 7:1; Wakolosai 3:5) Unapojiingiza katika mazoea hayo mabaya yanaweza kuleta athari mbaya kama uharibifu,umaskini, kutoaminiana, kuvunjika kwa familia, matatizo ya kiakili na kihisia, magonjwa na kifo cha mapema.
Kwa wale wanaoishi kwa kufuata kanuni za Mungu wanakuwa na mahusiano mazuri, wanajiheshimu, na kuwa na Amani ya akili. Katika kitabu cha Isaya 48:17,18 inasema hivi “Bwana mkombozi wako, mtakatifu wa Israel asema hivi; mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;”
5.      KUONYESHA UPENDO USIO NA UBINAFSI.
“Na kwa habari ya vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga”.(I Wakorintho 8:1)
Tunachokiona hapa ni kuwa Upendo hujenga, Huweza kujenga mahusiano mazuri kati ya mtu na mtu pamoja na kuleta ushirikiano toka jamii moja na hadi nyingine. Na maana halisi ya Upendo ni kujitoa wewe mwenyewe bila ya uhakika kuwa upendo wako utarejeshwa . Kwa maana hiyo basi Upendo ni tendo la Imani  wala halihitaji kurudishwa.
“Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na Imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina Upendo, si kitu mimi. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabali; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote”. (I Wakorintho 13:2,4-7)
Upendo unaotajwa hapa si ule wa kimahaba ambao una mahali pake panapofaa. Badala yake ni upendo unaodumu ambao unaongozwa na kanuni za Mungu. Isitoshe, mtu haonyeshwi tu upendo huo bali anauonyesha kwa matendo.
Kwa wazazi, Upendo unamaanisha  kuwa na hisia nyororo kuwaelekea watoto wao na kuwapa mwongozo ulio wazi unaotegemea Biblia kuhusu maadili na tabia nyingine. Watoto wanaolelewa katika mazingira kama hayo hujihisi salama,Wanapendwa, na kuthaminiwa wakiwa sehemu ya familia iliyo imara.
Kwa wenzi walio na matatizo katika ndoa yao wanaamua kusoma pamoja maneno ya Yesu yanayopatikana kwenye Marko 10:9 yanayosema “Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe”. Sasa, lazima wajichunguze mioyo yao. Je wanashangilia pamoja na kweli za biblia? Je wataiona na kuitendea ndoa kama kitu kitakatifu, kama vile Mungu anavyoiona? Je wako tayari kujitahidi kutatua matatizo yao kwa upendo? Kwa kufanya hivyo wanaweza kufanya ndoa yao ifanikiwe na kuanza upya kufurahia Upendo ule wa mwanzo.
6.      TAMBUA UHITAJI WAKO WA KIROHO.
“Heri walio maskini wa roho, Maana ufalme wa mbinguni ni wao” (Mathayo 5:3). Wenye furaha ni wale wanaotambua uhitaji wao wa kiroho, tofauti na wanyama wanadamu wana uwezo wa kuthamini mambo ya kiroho. Tutatambua uhitaji wetu wa kiroho pale tutakapokuwa watu wa kutaka kujifunza maneno ya Mungu kila mara na kuomba zaidi, ndipo yule roho atakapomwagwa kwa wingi sana ndani yetu. Kumwagwa kwa roho wa Mungu kwa wingi kutaamsha hari ya kuifanya kazi ya Mungu kwa nguvu zote, akili zote na uwezo wote kisha twende nyumbani kuishi milele.
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu kristo uliyemtuma” (Yohana 17:3). Kumbe uzima wa milele unapatikana pale tunapomjua Mungu na kuitenda kazi yake hapa duniani.
              


No comments:

Post a Comment