Thursday, April 2, 2015

ALBINO NAYE NI MTU KAMA WENGINE.


ALBINO NAYE NI MTU KAMA WENGINE.
 
Neno Albino linamaanisha mtu mweupe, linatokana na neon la lugha ya kilatini –albus-lino maanisha  “-eupe”. Kuanzia karne ya 17 neno Albino limekuwa likitumika katika kueleza hali ya kundi la viumbe hai (watu, wanyama na hata mimea) ambao wana upungufu au ukosefu wa rangikatika ngozi, macho na nywele. Kwa binadamu ni bora kutumia maneno “Watu wanaoishi na ualbino kwani itamaanisha kuwa ni  watu kama wengine ila wanaishi na hali tofauti ya “ualbino”.
Lugha inajenga dhana na kuunda hali ya ukweli/uhalisi. Kwa sababu hiyo ni lazima tuache kutumia maneno  “zeruzeru”. Neno hili linamaanisha sifuri mara mbili au mtu asiye na thamani. Utumiaji  wa   neno hili ni dharau ya utu na kulaumu watu wanaoishi na ualbino kama kosa lao.
Albino wana ngozi nyeupe, nywele nyeupe au nyekundu na macho ya kijivu au ya bluu. Ngozi yao ni nyeupe zaidi kuliko ndugu zao wa familia moja au watu wa jamii yake ambao hawana hali ya ualbino. Ngozi hii inaonekana zaidi kuwa nyeupe katika familia za watu weusi, ingawaje, ualbino hutokea kwa watu wa kila taifa, rangi, kabilana dini. Albino wako katika mabara yote ulimwenguni.

Je ualbino unasababishwa na nini?                                                                                                                                                                     Watu wenye ualbino hawana uwezo kabisa au wana uwezo mdogo wa kuwa na rangi kwenye ngozi zao, nywele na macho. Rangi hii huitwa  “melanini”. Rangi ya ngozi itategemeana na kiasi cha melanini kilichopo. Hali ya kuzalisha melanini imekaa katika vinasaba vyetu. Kama vinasaba vya kutoa melanini havipo au vimebadilishwa madhara yake ni ukosefu au upungufu wa rangi. Kwa hiyo hali ya ualbino ni ya kurithi. Inaweza kurithishwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto.

Je ualbino unarithiwa vipi?                                                                                                                                                                                         
Watoto wengi wanaozaliwa na ualbino, wazazi wao wana rangi ya ngozi, nywele na macho inayofanana na watu wa kabila /asili yao. Mwili wa kila mwanadamu una seti mbili za vinasaba (moja hutoka kwa mama na moja hutoka kwa baba). Mtu anaweza kuwa na rangi ya asili ya kawaida lakini akawa na kinasaba cha ualbino. Kama mtuana kinasaba kimoja cha rangi ya asili na kimoja cha ualbinoatakuwa  na taarifa za vinasaba vya kutosha kutengeneza  rangi ya asili. Kinasaba cha ualbino ni seli dhoofu haiwezi peke yake kuonyesha ualbino mpaka mtu awe nazo mbili kwa pamoja.
Kama wazazi wote wawili wana vinasaba vya ualbino na wote hawaonyeshi ualbino, kuna uwezekano wa kupata mtoto Albino kati ya mmoja katika wanne kwa kila mimba.

Ni wanadamu tu pekee ndiyo wameathiriwa na ualbino?        
          
Hapana. Ualbino ni hali inayoweza kutokea kwa wanadamu na wanyama wa kundi la mamalia. Tembo weupe wa India hujulikana sana na walithaminiwa sana katika mahakama ya mfalme , vilevile chui, twiga na samba weupe ambao sasa wanafurahiwa sana kwenye bustani za wanyama na mbuga za wanyamapori.
Hapa Tanzania inakisiwa kuwa kuna Albino wapatao zaidi ya elfu kumi hivi, na kwa wingi wanapatikana katika maeneo ya mikoa ya kanda ya ziwa –Tanzania. Inakisiwa kwa mujibu wa tafiti katika nchi nyingine kama Nigeria na Afrika kusini kuwa kuna mtu 1 kati ya 4,000-5,000 ni albino na idadi hii ni kubwa sana ukilinganisha na Ulaya au  Marekani  ambapo ni wastani wa mtu 1 kati ya watu 15,000-20,000 hivi.







Watu wanaoishi na ualbino wanafanana wote?                                                                                                                                               Hapana. Albino wote hawafanani bali wanatofautiana kufuatana na kiasi cha melanini walicho nacho wengine hawana kabisa na wengine wanayo kwa kiasi kidogo tu. Wanasayansi wamegundua aina mbalimbali za ualbino. Kufuatana na aina hizi za ualbino wengine wana ngozi ya rangi ya kahawia nyepesi na nywele nyeupe, wengine wana ngozi nyeupe na nywele nyeupe, baadhi wana mabaka meusi machache kwenye ngozi nyeupe.

Nini matatizo ya macho ya Albino?                                                                                                                                                       Mboni katika macho ya Albino haina pigimenti ya rangi. Kwa hiyo ni rahisi macho yao kuathiriwa na mwanga. Kwani mboni ndiyo inayolinda jicho la ndani lisipatwe na mwanga mkali. Vilevile kama mboni inavyolinda jicho dhidi ya mionzi ya jua, inakuwa vigumu kuona kwa usahihi utofautikatika picha. Kwa hiyo uwezo wa kuona unatiwa mawingu mawingu. Hivyo basi ni muhimu sana kukwepa inavyowezekana mionzi ya jua na kulinda macho kwa kuvaa miwani ya jua. Albino mara nyingi hawaoni vizuri  na  hii inatofautiana kwa mmoja hadi mwingine. Inawezekana ni kutoona mbali,kutoona karibu au kuona mawingu mawingu. Matatizo haya hutofautiana katika albino. Ukweli ni kuwa albino anaweza kushiriki katika michezo mbalimbali, baadhi wanaweza  kuendesha magari  na wengi wanaweza kusoma maandishi ya kawaida.

Kwanini Albino wanawekwa katika kundi la walemavu? 

Ulemavu maana yake ni hitilafu katika mwili au akili inayomwekea mipaka mtu asiweze kufanikisha shughuli Fulani katika maisha yake. Albino wanatambuliwa kama watu wenye ulemavu hasa kwa ajili ya uwezo wao wa kutokuweza kuona vizuri. Dalili za kutokuwa na uwezo wa kuona vizuri hutofautiana kuanzia wale ambao hawaoni karibu, wasioweza kuona mbali na wale ambao wanashindwa kuona vizuri au kuona mawingu mawingu.
Pamoja na matatizo ya kuona, ngozi ya albino ni rahisi sana kudhurika kwa mionzi ya jua. Hatma yake ikiwa ni uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya ngozi. Hivyo basi kila albino anashauriwa daima kujikinga dhidi ya mionzi ya jua kwa kuvaa nguo za mikono mirefu, kuvaakofia pana, kuvaa miwani ya jua na kwa wale wenye uwezo kujipaka mafuta maalumu yanayosaidia kukinga ngozi dhidi ya mionzi ya jua.

Albino ni watu wa kawaida, je kisayansi hii ni kweli?                                                                      
Hii ni kweli kabisa. Watu wanaoishi na ualbino ni watu wa kawaida kama binadamu wengine wote na wanaweza kuwa wa aina tofauti kama binadamu wengine. Wanaweza kuwa wadogo au warefu, wanene au wembamba, warembo au wasio warembo, wenye vipaji au wa wastani. Wanaweza kuwa na uthubutu au wenye aibu, wachangamfu au jeuri, wenye tabia ya ushirikiano au wenye tabia ya uhasama.
Kumbuka kuwa utofauti  wao upo tu kwenye muonekano wa ukosefu wa rangi kwenye ngozi, nywele na macho. Wakati umefika jamii kujifunza kuwakubali albino kama binadamu wengine, wenye hisia, mahitaji, uwezo na wanastahili haki zote za binadamu kama alivyo mtu mwingine yeyote.

Albino anaweza kuwa na maisha ya kawaida na yenye mafanikio katika maisha? 
     
Imani iliyojengeka kwenye jamii kuwa albino wana uwezo mdogo si ya kweli. Ipo mifano mingi ya watuwalioweza kupata mafanikio katika maisha ambao pia ni albino. Wapo ambao ni waalimu, wanasayansi, wanasheria, na wengine wapo kwenye siasa na uongozi. Mwanamuziki wa kimataifa kutoka nchi ya Mali anayeitwa Salif Keita amefikia mafanikio makubwa sana duniani kote kuanzia bara la Afrika na Ulaya kiasi cha kuitwa “Sauti ya dhahabu”. Yeye alizaliwa katika familia ya muasisi wa taifa la Mali  Sundiata keita. Hii inadhihirisha kuwa albino anaweza kuzaliwa katika familia yeyote kuanzia zile za kifalme na hata familia maskini za wakulima wadogo wadogo.
Je zipo sheria zinazolinda watu wenye ulemavu hapa Tanzania?                                                                                                              Ndiyo zipo sheria hapa Tanzania zinazowalinda watu wenye ulemavu, Tanzania ilitia saini na kuridhia mkataba wa kimataifa wa ulinzi, haki na usawa kwa watu wenye ulemavu mwaka 2006. Kwa kitendo cha kuridhia mkataba huo wa kimataifa Tanzania imeonyesha nia yake ya kuwalinda na kudumisha haki za watu wenye walemavu.  Hata katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977(Kama ilvyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inakataza ubaguzi wa aina yeyote kwa watu wenye ulemavu.
Zipo sheria nyingi zinazolinda haki na usawa kwa walemavu ambazo zinahusika na sekta mbalimbali kwa mfano; elimu na mafunzo, ajira(sheria ya watu wenye ulemavu  Na.2   ya mwaka 1982, matunzo(kanuni za ajira za watu wenye ulemavu Na. 3  ya mwaka 1985, na ustawi(sheria ya matunzo ya watu wenye ulemavu  Na.3  ya mwaka 1982. Ipo pia sera ya taifa kuhusu ulemavu ya mwaka 2004(Sheria ya haki na upendeleo kwa watu wenye ulemavu  Na.9   ya mwaka  2006, na hii ni kwa Zanzibar tu.

JE, ZIPO SHERIA ZINAZOLINDA HAKI ZA ALBINO? 
    
Haki za msingi za albino zinalindwa chini ya katiba ya nchi pamoja na sheria zinazohusika na sekta mbalimbali. Sheria hizi zinakataza na kukemea aina zote za ubaguzi kwa misingi ya rangi, kabila, ulemavu na kadhalika.
Sera ya taifa ya ulemavu inabainisha hali yan ulemavu kuwa ni, “kutokuwa au kupungukiwa na uwezo wa kushiriki kwa usawa katika shughuli  za kawaida za kijamii kutokana na sababu za mapungufu ya kimwili, kiakili au kijamii”. Sera hiiinatoa mwongozo wa kutolewa  kwa haki na fulsa sawa kwa walemavukupata mambona huduma za msingi kama  elimu, taarifa, ajira, matunzo huduma za afya, kumudu na kufikia huduma muhimu. Katika siku za karibuni kumeongezeka vitendo vya kikatili dhidi ya albino ambavyo ni pamoja na mauaji ya kikatili na kukatwa viungo kutokana na imani za kishirikina. Watu wenye ualbinowanalindwa kisheria kutokana na vitendo hivi kwa kupitia sheria zilizopo za makosa ya jinai. Serikali pia imechukua hatua za kudhibiti hali hii isiendelee kutokea ikiwa ni pamoja na kuanza kuwaandikisha rasmi (kufanya sense) watu wenye ualbino, na pia kuanzishwa kwa ulinzi kwa Albino kupitia jeshi la polisi na jamii kwa ujumla.
Mpaka sasa kunajitihada zinazofanywa na serikali hasa katika utungwaji wa sera  ila wakati Fulani kuna kulegalega katika usimamizi wa sera hizo, kwa baadhi ya watu wasio waaminifu kuchukua muda mrefu kufuatilia kesi hizi, ili hali kuna ushahidi pasipo shaka katika tuhuma hizo. Na wengi wa watu wanaofanya vitendo hivi vya ukatili ni pamoja na baadhi ya  wafanyabiashara vigogo, watu mashuhuri katika jamii, na baadhi ya vigogo katika mamlaka, kwa imani potofu kuwa ili waendelee kufanikiwa zaidi ni lazima wawapelekee hao waganga wa kienyeji baadhi ya viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi. Ebu fikiria kidogo kwa akilia ya kawaida tu, kwani yeye anayekwambia hivyo yeye hapendi kuwa na maisha mazuri?, mbona yeye anaishi katika makaazi ya tope leo kesho linaanguka ? inamaana yeye hataki kufanikiwa kimaisha?, baada ya kujiuliza maswali hayo tambua kuwa vitu vya masharti ya kuleta viungo vya hawa albino mwisho wake ni kuitaka roho yako iwe kama sadaka kwa miungu yao.
Wakati umefika sasa kama ilivyofanywa kwa janga la ukimwi kwa kuanzisha mitaala mashuleni na vyuoni , pia ukatili huu wa kuwaua maalbino utangazwe kama janga la taifa na zichukuliwe hatua mahususi na mbinu mbadala ili kukomesha tatizo hili, lakini pia kwa upande wa jeshi la polisi nchini kuna baadhi ya watumishi wanaoshirikiana na wahalifu hawa wa mauaji ya albino, kwa kupoteza ushahidi makusudi nao wachukuliwe hatua pindi wanapobainika, maana tunaweza kuwaamasisha wananchi katika mapambano haya ila ikaja kuonekana ni sawa na kumchezea mbuzi gitaa ili acheze wakati hawezi kucheza muziki huo.
Tumeuanza mwaka mwingine tena , tena wenye purukushani nyingi kuelekea uchaguzi mkuu wa MADIWANI, WABUNGE NA URAIS , BAADHI YAO WATATAPELIWA NA KUDANDANYWA KULETA VIUNGO VYA MAALBINO ILI KUFANIKIWA KUINGIA MADARAKANI, Ukweli ni kwamba unajitengenezea laana wewe na familia yako isyokuwa na hatia, na kushindwa utashindwa tu. Haiwezekani kuiondoa roho ya mtu nawe ukabaki salama mbele za mwenyezi MUNGU.

No comments:

Post a Comment